Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi kote nchini kuwagomea madereva wazembe na kutopanda magari yao ili kuepuka ajali lakini pia amewataka wananchi hao kutoa taarifa juu ya madereva hao kwa vyombo vya usalama. Mama Samia amesema hayo leo alipokuwa kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya usalama barabarani, yaliyofanyika katika viwanja vya Mashujaa Moshi mkoani Kilimanjaro na kuwaambia wananchi kuwa wana haki ya kugoma kupanda kwenye magari ambayo madereva wake ni wazembe. "Ni haki yenu na jukumu lenu kuwasusia madereva wazembe na kuwagomea kupanda magari yao" alisema Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan. Mbali na hilo Makamu wa Rais ameviagiza vyombo vya usalama barabarani kuakikisha kwamba kila dereva anakuwa na leseni halali na aliyoipata kwa njia halali na si leseni za kununua bila kupita katika masomo pia ametaka leseni feki zikamatwe zote kwani anaamini zipo nyingi mtaani.